Baada ya kushehereka na Sikukuu ya krismasi na kuukaribisha mwaka 2012 Kidarubini kimekuja na Chekelea Time itakayokuwa inawajia mtandaoni kwa njia ya kushtukiza kwee kwee kwee!!Leo somo la Chit-Chat linahusu methali ambazo wengi wetu tutakuwa tunazikumbuka vizuri.
Mwalimu: Simameni!
Wanafunzi: Shikamoo mwaaaa--limu.
Mwalimu: Kaeni.
Wanafunzi: Asante mwaaaa--limu.
Mwalimu: Haya, leo ninataka nijue nani anazikumbuka methali tulizojifunza jana. Mwenye kufahamu anyooshe kidole juu. Penye kuku wengi...?
Kipensi ananyoosha kidole.
Mwalimu: Kipensi, malizia methali.
Kipensi: Penye kuku wengi chagua mmoja awe kitoweo!
Mwalimu: Mh!!! Haya, methali ya pili. Mtoto akililia wembe...?
Kisistimu ananyoosha kidole.
Mwalimu: Haya Kisistimu malizia methali.
Kisistimu: Mtoto akililia wembe atakuwa kinyozi!
Mwalimu: Duh! Haya tuendelee. Asiyesikia la mkuu...?
Kiroba ananyoosha kidole.
Mwalimu: Haya Kiroba, malizia methali.
Kiroba: Asiyesikia la mkuu, itakuwa sio mwanae wala hawana uhusiano!
Mwalimu: Nauliza methali ya mwisho, sitaki jibu la ovyo vinginevyo nitawapatia adhabu darasa zima. Mbio za sakafuni...?
Kipensi ananyoosha kidole.Mwalimu: Haya Kipensi jibu.
Kipensi: Mbio za sakafuni, hazimo hata kwenye olimpiki!!
Mwalimu: Dah!! Acha tu nirudi kijijini nikalime.
No comments:
Post a Comment